Jumamosi 31 Januari 2026 - 23:00
Vita dhidi ya Iran ni vita vya ukafiri dhidi ya utawala wa Kiislamu/ Jamhuri ya Kiislamu itasalia imara hadi iikabidhi bendera kwa Imam Mahdi (as)

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, huku akisisitiza kuwa makabiliano ya sasa dhidi ya Iran kimsingi ni makabiliano kati ya ukafiri na utawala wa Kiislamu, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasalia imara na thabiti hadi pale itakapokabidhi bendera kwa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake).

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, siku ya Ijumaa tarehe 30 January, alitoa khutba za Swala ya Ijumaa mjini hapo katika Husayniyya Kuu ya Fatimiyya.

Katika khutuba zake Imam huyo, alizungumzia suala la uteuzi wa Nouri al-Maliki kugombea wadhifa wa Waziri Mkuu wa Iraq na msimamo wa Marekani kuhusu jambo hilo, akautaja kuwa ni “kuvunja na kudharau uamuzi wa taifa la Iraq.” (1) Alisisitiza kuwa msimamo huo ulisababisha hisia na radi amali kubwa miongoni mwa wasomi, vyama vya kisiasa na wananchi wa kawaida, kwa sababu ilikuwa ni kuingilia mipaka na uhuru wa kitaifa wa Iraq.

Katika muktadha huo huo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji aliitaja kauli za Donald Trump, Rais wa Marekani, kuwa ni “zisizo na adabu,” na akatoa wito wa kuheshimu misingi ya adabu na diplomasia ya kisiasa.

Alisisitiza kuwa: Iraq si kama baadhi ya nchi za eneo ambazo Trump huzitaja kuwa “ng’ombe wa kukamuliwa.” Akitilia mkazo kuwa “Iraq si taifa linalokubali udhalili, bali lina dhamira isiyovunjika,” alisema kuwa; kuhusu chaguo lililopo mbele ya muungano wa Mfumo wa Uratibu uliomteua Nouri al-Maliki, unakabiliwa na njia mbili: ima wajiondoe katika uamuzi wao—ambalo litamaanisha kukubali kupoteza uhuru wa kitaifa—au walisimamie suala hilo kwa njia ya kidiplomasia.

Vita dhidi ya Iran ni vita vya ukafiri dhidi ya utawala wa Kiislamu

Katika sehemu ya masuala ya kikanda, Imam wa Ijumaa wa Najaf, huku akirejelea harakati za meli za kivita za Marekani kuelekea Ghuba ya Uajemi na vitisho vya Washington dhidi ya Iran, alisema:
“Vita hivi ni vita kati ya Ukafiri na utawala wa Kiislamu.”

Imam wa Ijumaa wa Najaf alitathmini pia uzoefu mbalimbali ulioshindikana wa Marekani katika kujaribu kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran—uzoefu ambao wa mwisho ilikuwa ni vita vya siku 12 na baada yake fitna za ndani [ambapo mawakala wa nguvu za kigeni, zikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni, hasa katika siku za 18 na 19 ya mwezi Dey, walizua machafuko]. Akibainisha kuwa katika vipindi hivyo Israel na Marekani walishindwa, na kwamba leo Marekani imeingia moja kwa moja uwanjani, alisisitiza: “Tunaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaanguka mpaka pale itakapoikabidhi bendera kwa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake),” na akauelezea msimamo huo kuwa ni “utabiri wa kisasa wa ulimwengu wa leo.”

Katika khutba ya kidini, alizungumza kuhusu fadhila za kumzuru Imam Husayn (a.s.) ndani ya nusu ya Shaaban, pamoja na kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake).

Kisha akarejelea matukio ya Intifadha ya Shaaban ya mwaka 1991 Miladia, ambapo majimbo 14 ya Iraq yaliokolewa kutoka mikononi mwa Chama cha Baath, chama ambacho kilikuwa kikipaza kauli ya “leo hakuna Shia aliyopo.” (2)

Imam wa Ijumaa wa Najaf alisisitiza kuwa: “Leo tunaishi kwa baraka ya damu ya mashahidi hao; intifadha hiyo iliweza kubadilisha mizania ya kimataifa na ikawa mwanzo wa kushuka kwa rehema za Mwenyezi Mungu, hadi hatimaye mwaka 2003 tuliposhuhudia kuanguka kwa mtawala dhalimu na chama chake."

(1)Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Donald Trump, Rais wa Marekani, hapo awali kupitia jukwaa la "Truth Social" aliukosoa vikali mchakato wa uteuzi wa Nouri al-Maliki kuwa Waziri Mkuu wa Iraq, akiandika: “Nimesikia kwamba nchi kubwa ya Iraq huenda ikafanya uamuzi mbaya sana wa kumrudisha Nouri al-Maliki katika nafasi ya Uwaziri Mkuu…” na akaongeza kwa vitisho: “Iwapo atachaguliwa, Marekani haitatoa msaada wowote kwa Iraq… Iraq bila msaada wa Marekani haina nafasi ya kufanikiwa.”

(2) Intifadha ya Shaaban, ulikuwa ni uasi wa wananchi wa Iraq dhidi ya utawala wa Saddam Hussein. Ilifanyika katika mwezi wa Shaaban mwaka 1411 Hijria (sawa na 1991 Miladia). Uasi huo ulianza Basra na ndani ya siku 15, majimbo 14 kati ya 18 ya Iraq yaliangukia mikononi mwa waasi. Chama cha Baath kilikandamiza vikali uasi huo, hali iliyosababisha kuuawa kwa makumi ya maelfu ya watu na kuwafanya karibu watu milioni mbili kuwa wakimbizi. Serikali ya wakati huo ilishambulia kwa mabomu Haram ya Amir al-Mu’minin Imam Ali (a.s.) na Haram ya Imam Husayn (a.s.), ikawakamata wanazuoni na wanafunzi wengi wa dini na kuwaua wengi wao, isipokuwa walioweza kukimbia Iraq.
Vilevile, shule nyingi za kidini, misikiti na husayniyya ziliharibiwa na utawala wa Baath.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha